Showing posts with label Safari. Show all posts
Showing posts with label Safari. Show all posts

Thursday, March 29, 2018

Kitabu Kinaendelea Kupigiwa Debe Nebraska

Mfanya biashara au mtoa huduma hufarijika anapoona wateja wakija tena kufuata kile walichokipata kabla. Imekuwa hivyo kwangu kama mwandishi. Mimi si mfanyabiashara, bali ni mwalimu. Uandishi ni sehemu ya ualimu. Ninafarijika na kufurahi ninapoona watu wakifaidika na maandishi yangu.

Ninaandika ujumbe huu kuelezea ujumbe juu ya kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kutoka Nebraska, jimbo mojawapo la Marekani. Waumini wa kanisa la ki-Luteri la Marekani, ELCA, wa sinodi ya Nebraska wana programu ya kuzuru Tanzania iitwayo vision trip, kujifunza masuala ya utamaduni na maisha ya wa-Tanzania na kubadilishana uzoefu, ili kujenga mahusiano na maelewano.

Mwaka hadi mwaka, waratibu wa programu wamekipendekeza kitabu changu hicho. Leo nimeona chapisho la mwongozo kwa ajili safari ya mwaka 2018. Humo, kama ilivyokuwa miaka iliyopita, kitabu changu kimeendelea kupendekezwa kwa wasafiri:

For those persons wanting to more deeply explore cultural differences between Africans and Americans, the book Africans and Americans by Joseph Mbele is recommended. This book is available at: www.africonexion.com

Tafsiri kwa ki-Swahili:

Kwa wale wanaotaka kufuatilia zaidi tofauti za tamaduni baina ya wa-Afrika na wa-Marekani, kitabu "Africans and Americans" cha Joseph Mbele kinapendekezwa. Kitabu hiki kinapatikana www.africonexion.com


Ninafurahi na kushukuru kwamba watu wanaona umuhimu wa kitabu hiki. Kingekuwa hakina manufaa, wangeacha kukipendekeza tangu zamani. Niliwahi kukutana na baadhi ya hao wasafiri wa Nebraska katika safari ya kwenda Tanzania wakiwa na kitabu changu, kama nilivyoandika katika blogu ya ki-Ingereza. Ninafurahi kuwa kitabu changu kinasaidia lengo la kujenga maelewano baina ya wa-Tanzania na wa-Marekani.

Wednesday, January 11, 2017

Zawadi Kutoka Ramble Pictures Kwa Heshima Ya Hemingway

Wiki iliyopita nimepata zawadi ya picha kutoka Ramble Pictures, kampuni ya kutengeneza filamu. Kampuni hiyo ndiyo iliyotengeneza filamu ya Papa's Shadow, inayohusu maisha na safari za mwandishi maarufu Ernest Hemingway Afrika Mashariki, pamoja na maandishi yake kuhusu Afrika Mashariki. Sehemu kubwa ya filamu hiyo ni mazungumzo baina ya Mzee Patrick Hemingway na mimi, kuhusu masuala hayo.

Picha niliyopewa inaitangaza filamu ya Papa's Shadow. Inamwonesha Ernest Hemingway, Patrick Hemingway na mimi, Kuna pia Mlima Kilimanjaro na nchi tambarare chini ya mlima, na pia ndege ikiwa angani. Hiyo picha ya mlima na mazingira yake, pamoja na ndege, inakumshia hadithi maarufu ya Hemingway, "The Snows of Kilimanjaro."

Nimeguswa na picha hii. Ni heshima kubwa kuliko ninavyostahili kuwekwa sambamba na Ernest Hemingway na Patrick Hemingway. Ernest Hemingway alileta mapinduzi katika uandishi na alitunukiwa tuzo ya Nobel katika fasihi mwaka 1954. Patrick Hemingway ni mtu muhimu kwa watafiti wa Hemingway, akiwa ni mtoto pekee aliye bado hai wa Ernest Hemingway. Ametoa na anaendelea kutoa mchango mkubwa wa kuhariri maandishi ya Hemingway na kuyaandikia utangulizi.

Kwa upande mwingine ninafurahi kuoneshwa pamoja na Patrick Hemingway, ambaye ni mtu wa karibu kwangu. Ananifundisha mengi kuhusu Afrika Mashariki ya wakati alipoishi kule, kuhusu maisha na uandishi wa Hemingway, na kuhusu waandishi wengine, hasa wa wakati wa Hemingway.

Vile vile, Patrick Hemingway anakipenda sana kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Hata katika filamu ya Papa's Shadow, anakitaja, na kuna mahali anasoma kisehemu cha kitabu hiki kwa ki-Swahili na tafsiri yangu ya ki-Ingereza.

Filamu ya Papa's Shadow inaelezea upande wa Ernest Hemingway ambao haufahamiki vizuri, yaani jinsi alivyovutiwa na Afrika kwa maisha yake yote. Katika kufanya utafiti juu ya Hemingway na kusoma maandishi yake kwa miaka kadhaa, niligundua kuwa aliipenda Afrika tangu alipokuwa mtoto. Ndipo nikaamua kutunga kozi kuhusu mada hiyo.

Mwanafunzi mmoja katika kozi hiyo, Jimmy Gildea, alipata motisha ya kutengeneza filamu, na matokeo yake ni Papa's Shadow. Pamoja na kuelimisha juu ya uhusiano wa Hemingway na Afrika, filamu hii inaitangaza Tanzania. Nakala za filamu hii zinapatikana kwa kuwasiliana na Ramble Pictures kwa barua pepe: info@ramblepictures.com au kwa simu (952) 426-5809.

Thursday, December 1, 2016

Maandalizi ya Wanachuo wa Gustavus Adolphus Waendao Tanzania

Jana nilipata ujumbe kutoka kwa Profesa Barbara Zust wa Chuo cha Gustavus Adolphus akiulizia iwapo nitaweza kwenda kuongea na wanafunzi wanaojiandaa kwenda naye Tanzania kwa safari ya kimasomo. Ameniambia kuwa watakuwa na kikao cha maandalizi ya safari tarehe 2 na 3 Januari, katika kituo cha mikutano cha Mount Olivet. Nimefanya mazungumzo hayo tena na tena miaka iliyopita.

Katika ujumbe wake, Profesa Zust amekumbushia kuwa, kama ilivyo jadi, wanafunzi hao watakuwa wameshasoma kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Pia amekumbushia jinsi wanafunzi wanavyoshukuru na kufurahia kwamba wanapokuwa Tanzania wanakutana na yale ambayo ninakuwa nimewaeleza kitabuni na katika mazungumzo.

Taarifa hii ni muhimu kwangu, na ndio maana ninaiweka hapa katika blogu yangu, kama kumbukumbu. Kwa kuzingatia umuhimu wa suala hili, nimeitika mwaliko wa Profesa Zust na kumwambia kuwa nitakwenda kukutana nao tarehe 2 Januari. Kama kawaida, panapo majaliwa, nitaandika taarifa katika blogu hii.

Thursday, September 8, 2016

Wasomaji Wangu Wa Nebraska Waendao Tanzania

Nina jadi ya kuwaongelea wasomaji wangu katika blogu hii, kama njia ya kuwaenzi. Ni jambo jema kwa mwandishi kufanya hivyo. Leo ninapenda kuwakumbuka wasomaji wangu wa sinodi ya Nebraska ya Kanisa la Kiluteri la Marekani, ambao tangu zamani wamekuwa na programu ya kupeleka watu Tanzania kuendeleza uhusiano baina yao na wa-Luteri wa Tanzania.

Hao wasafiri, sawa na wenzao wa sinodi zingine za Marekani, wamekuwa wakitumia kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences katika kujiandaa kwa safari, ili kuzielewa tofauti za tamaduni za Marekani na Afrika. Ni elimu muhimu katika ulimwengu wa utandawazi wa leo, ambayo nje ya ufundishaji wa darasani, ninashughulika nayo.


Wakati huu ninapoandika, waumini wa Nebraska wanajiandaa kwa safari ya Tanzania, ambayo itafanyika mwezi Februari mwaka 2017. Wameitangaza safari hii mtandaoni, na mratibu mojawapo wa safari, Martin Malley, ameniandikia ujumbe leo akisema, "We still recommend your book." Katika ukurasa wa 16 wa chapisho la maelezo na maandalizi ya safari, kitabu hicho kimetajwa.

Ninapowakumbuka wasomaji wangu wa Nebraska, ninakumbuka nilivyokutana katika uwanja wa ndege wa Amsterdam na kikundi cha watu wa Nebraska waliokuwa wanakwenda Tanzania, tukasafiri pamoja. Mimi sikuwajua, ila wao walinitambua, kama nilivyoelezea katika blogu yangu ya ki-Ingereza.


Saturday, September 26, 2015

Nimehojiwa Kuhusu Hemingway na "Papa's Shadow"

Leo nimekuwa na mahojiano na mwandishi wa gazeti la Manitou Messenger linalochapishwa hapa chuoni St. Olaf. Ni gazeti la wanafunzi, ambalo limekuwa likichapishwa kila wiki kwa miaka 125. Mahojiano yetu yalikuwa juu ya filamu ya Papa's Shadow. Katika ujumbe wa kuomba mahojiano, mwandishi aliandika:

...we are doing a feature article this week on the documentary, Papa's Shadow and Ramble Pictures. We learned that you were instrumental in the inspiration for and production of this film, and we were hoping you could answer a few quick questions.

Katika mahojiano, tumeongelea nilivyoanza kuvutiwa sana na mwandishi Ernest Hemingway, nilipoombwa na Thomson Safaris kuongoza msafara mkubwa wa wanafunzi, wazazi na walimu, katika safari ya Tanzania mwaka 2002. Hatimaye, baada ya miaka mitano ya kusoma maandishi na habari za Hemingway, nilitunga kozi Hemingway in East Africa, kwa ajili ya Chuo cha Colorado.

Baadaye, niliona niunde kozi hiyo kwa ajili ya wanafunzi wa Chuo cha St. Olaf. Nilifanya hivyo mwaka 2012. Wakati wa kuandikisha wanafunzi, alinifuata kijana aitwaye Jimmy Gildea, akaniomba nimruhusu kujiunga na kozi, kwa kuwa alimpenda Hemingway na alitaka kurekodi filamu ya kozi. Nilimsajili katika darasa.

Kozi ilikwenda vizuri, kama nilivyoandika hapa. Baada ya kurejea tena Marekani, baadhi yetu tulifunga safari ya jimbo la Montana kuonana na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliyebaki wa Ernest Hemingway. Tuliongea naye sana.

Jimmy alikuwa amenirekodi ofisini mwangu nikizungumza juu ya Hemingway, akachanganya mazungumzo haya na yale tuliyofanya na Mzee Patrick Hemingway,na akaongezea mambo mengine aliyorekodi Tanzania. Kwa bahati nzuri, tulipomaliza kozi, familia ya Jimmy walikuja kumchukua wakaenda kupanda Mlima Kilimanjao. Papa's Shadow inaonyesha safari yao ya kupanda mlima. Ni rekodi nzuri sana. Ninaamini itawavutia watalii.

Kuna mambo mengine niliyomwambia huyu mwandishi wa Manitou Messenger. Hasa, nilisisitiza azma yangu ya kuendelea kufanya kila juhudi kuuelimisha ulimwengu juu ya namna Hemingway alivyoipenda Afrika na namna maisha yake na fikra zake zlivyofungamana na Afrika. Nilimwambia pia kuwa Jimmy ni mfano murua wa kuigwa na wahitimu wengine wa vyuo. Alifuata na anaendelea kufuata anachokipenda moyoni mwake, yaani kutengeneza filamu za kuelimisha. Yeye na vijana wenzake katika Ramble Pictures wanajituma kwa roho moja katika shughuli zao na hawatetereshwi na magumu au vipingamizi vyovyote.

Thursday, September 24, 2015

"Papa's Shadow" Yapongezwa na Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa

Tarehe 20 mwezi huu nilipeleka ujumbe Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa kuhusu filamu ya Papa's Shadow. Sikuandika ujumbe mrefu, bali niliwatumia kiunganishi hiki.

Bila kuchelewa, tarehe 22 nilipata ujumbe kutoka kwao, ukiwa umeandikwa na Ndugu Noel Kabanda. Uwakilishi unaafiki kuwa Papa's Shadow ni "fursa maridhawa ya kuitangaza Tanzania ulimwenguni" na unasisitiza kuwa "Serikali inatambua mchango wa sanaa katika kuitangaza Tanzania katika sekta mbali mbali ikiwemo utalii na utamaduni."

Kwanza, kwa kuzingatia uwingi wa majukumu yanayowakabili wawakilishi wetu katika balozi zetu, nimeona ni muhimu kusema nilivyoguswa na jinsi Uwakilishi ulivyoushughulikia ujumbe wangu.

Pili, ujumbe wa Uwakilishi unawatia moyo wahusika wa Ramble Pictures, ambao ndio watengeneaji wa Papa's Shadow. Timu nzima ya Ramble Pictures ni vijana wa ki-Marekani, na baadhi yao walikuja Tanzania mwaka 2013 kwenye kozi yangu ya Hemingway Katika Afrika Mashariki. Ni furaha kwangu, na jambo la kujivunia, kuwaeleza vijana hao kuwa Uwakilishi wa Kudumu waTanzania Umoja wa Mataifa umeipokea Papa's Shadow kwa namna hii.

Papa's Shadow si filamu ya maigizo. Ni filamu ya kuelimisha kuhusu mwandishi Ernest Hemingway. Sehemu kubwa ya filamu hiyo ni maongezi baina yangu na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliyebaki wa mwandishi Hemingway. Tunaongelea maisha ya Hemingway, safari zake, uandishi wake, na fikra zake kuhusu masuala mbali mbali. Tunawafungua macho walimwengu kuhusu namna Hemingway alivyoipenda Afrika na alivyokuwa mtetezi wa Afrika.

Hemingway alisafiri na kuishi Afrika Mashariki mara mbili, mwaka 1933-34 na 1953-54. Aliandika hadithi, insha, barua na maandishi mengine ambayo ni hazina kubwa. Wenzetu katika nchi zingine ambako Hemingway alipita au kuishi na akaandika habari za huko, wametumia fursa hiyo kujitangaza, na wanawavutia watalii wengi sana. Mifano ni miji kama Paris (Ufaransa), Havana (Cuba), Oak Park (Illinois, Marekani), Key West (Florida, Marekani), na Pamplona (Hispania). Hemingway anapendwa ulimwenguni kote ambako watu wana utamaduni wa kusoma vitabu. Sina shaka kuwa Papa's Shadow italeta msisimko wa aina hiyo kwa kuwaelekeza mashabiki wa Hemingway nchini kwetu.

Hamu ya kuona Tanzania inafunguka macho kuhusu fursa hii ilinihamasisha kufanya utafiti juu ya safari za Hemingway katika nchi yetu na maandishi aliyoandika. Kozi niliyotunga ilikuwa na lengo hili. Nilitaka pia kuwasaidia walimwengu kuelewa umuhimu wa Afrika katika maisha na uandishi wa Hemingway. Kwa msingi huo huo, nilishiriki kikamilifu katika kufanikisha filamu ya Papa's Shadow.

Nimeeleza hayo yote ili kuweka wazi umuhimu wa ujumbe wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa. Ni mfano wa mshikamano unaotakiwa baina yetu wanadiaspora, serikali, na wananchi wenzetu.

Wednesday, December 17, 2014

Mwaliko Mwingine

Leo nimepata mwaliko mwingine wa kwenda kuzungumza na wanachuo wa chuo cha South Central ambao wanajiandaa kwa safari ya masomo Afrika Kusini. Mwaliko umetoka kwa mwalimu wao, Becky Djelland Davis. Hii ni mara pili yeye kunialika. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka jana, naye baadaye aliandika kuhusu mazungumzo yale katika blogu yake.

Nami nimeguswa kwa namna alivyoniandikia leo:

I will be taking students to South Africa again in May. This coming semester, we will again be reading your book Africans and Americans. I hope that perhaps you can talk with my students again? They loved you last time!

Huu ni mwaliko wa tatu kwa siku za hivi karibuni, na yote inangojea utekelezaji katika miezi michache ijayo. Wa kwanza niliuelezea hapa, na wa pili hapa. Mialiko hii ninayopata sio jambo jepesi au la mteremko. Inahitaji tafakari katika kujiandaa ili nitoe mawazo na mitazamo ya kiwango kinachokidhi mahitaji ya hao wanaonialika, na bora zaidi ni kufanya vizuri kuliko wanavyotegemea.

Hiyo inawezekana kutokana na juhudi ya kutafiti na kutafakari mambo kwa kina na upeo mpana zaidi ya yale yaliyomo katika kitabu changu, ambacho ndicho kinachochea hii mialiko. Sijioni kama ni mtaalam, bali mtafutaji wa elimu.

Kwa kuhitimisha, sherti nikiri kuwa ninafurahi kuona kuwa watu walionialika kabla wanaendelea kufanya hivyo, nami siwezi kuwaangusha. Hii ndio habari moja muhimu ya leo, ambayo nimeona niiwekee kumbukumbu katika blogu yangu hii.

Friday, August 5, 2011

Mitaani Mbamba Bay

Agosti tarehe 2 nilisafiri kutoka kijijini kwangu Lituru nikapitia Mbinga, na kufika Mbamba Bay, mwambao wa Ziwa Nyasa kwa matembezi.

Mbamba Bay, ingawa mji mdogo sana, unavutia kwa utulivu wake na mazingira, ukiwa ufukweni mwa Ziwa linalomeremeta kwa maji yake maangavu, kama nilivyowahi kuandika hapa.

Nilikuwa na bahati kwamba tarehe 3 Agosti ilikuwa siku ya jua na hali ya hewa ya kuvutia sana. Nami nilitumia fursa hii vilivyo. Niliteremkia ufukweni kufurahia upepo mwanana na mandhari murua ya Ziwa.


Kukaa nje ya nchi yako kunakupa mtazamo tofauti wa masuala ya nchi yako. Kwa mfano, hapa Tanzania, watoto wetu wana uhuru sana wa kucheza na kuzunguka mitaani, tofauti na Marekani, ambako watoto huangaliwa sana muda wote na wazazi au walezi wao, kwani si salama kuwaacha watoto bila uangalizi. Wa-Marekani wanaokuja huku kwetu wanashangaa wanapowaona watoto wakijizungukia wenyewe mitaani, raha mstarehe. Nimeongelea tofauti hizo katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Joto la Mbambay ni kishawishi kikubwa cha kutafuta sehemu ya kujipatia kinywaji baridi. Nami nilisogea baa hii iitwayo Bush House, nikatuliza kiu.



Hali ya Mbamba Bay ni ya utulivu usio kifani. Ni mahali pazuri kwa mapumziko. Kadiri siku zinavyopita, nina imani kuwa Mbamba Bay patakuwa kivutio kikubwa kwa watalii wa nje na ndani ya nchi. Nami niliamua kufika Mbamba Bay ili kupiga picha nichangie katika kuitangaza sehemu hii ya Tanzania.










Tuesday, June 28, 2011

Naenda kwa wa-Nyakyusa

Hivi karibuni, nitakuwa Tanzania na wanafunzi katika programu ya masomo inayoendeshwa na vyuo kadhaa vya Marekani kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kabla ya kuwafikisha Chuo Kikuu Dar es Salaam ambapo watasoma kwa muhula mmoja, nitakuwa nao maeneo ya nyanda za juu, hasa Iringa. Lakini, katika kupanga safari hii, nimeamua kuwafikisha hadi Mbeya na Ziwa Nyasa, wakaone na kujifunza. Iringa naifahamu vizuri, ila Mbeya nilipita tu mara moja, miaka ya mwisho ya sabini na kitu.

Wakati nangojea kwenda Mbeya, nawazia utamaduni wa wa-Nyakyusa. Mimi kama mtafiti, nimesoma kiasi kuhusu masimulizi yao ya jadi. Ninakumbuka maandishi ya watafiti kama Monica Wilson. Nina kitabu kiitwacho The Oral Literature of the Banyakyusa, kilichoandikwa na Christon S. Mwakasaka. Nadhani nilikinunua Dar es Salaam, nikawa nakisoma mara moja moja.

Lakini wakati huu ninapongojea safari ya Mbeya, kitabu hiki kinanivutia kwa namna ya pekee. Kina hadithi za jadi, lakini vile vile nyimbo na tungo zingine zinazoelezea mambo ya hivi karibuni ya historia na siasa u-Nyakyusa na Tanzania kwa ujumla.

Natafuta maandishi mengine ya kuongezea ufahamu wangu. Kwa hilo naweza kusema nimeathiriwa na wa-Marekani. Wao, kabla ya kusafiri, wana hiyo tabia ya kusoma habari za sehemu waendako. Ni jadi nzuri. Kusafiri kunatupanua akili, lakini kusoma habari za tuendako kunautajirisha zaidi ufahamu wetu.

Thursday, September 16, 2010

Kwa Nini Ninablogu

Wiki kadhaa zilizopita, wanablogu watatu tulikutana Sinza, Dar es Salaam, tukaongea kuhuau masuala mbali mbali. Kati ya mambo mengi, tuliondoka na suali: kwa nini tunablogu? Bofya hapa. Baada ya kulitafakari suali hili kiasi, napenda kuelezea kidogo kwa nini ninablogu.

Kwanza, nakumbuka kuwa nilianza kublogu baada ya kuhamasishwa na ndugu Freddy Macha na Jeff Msangi, mmiliki wa Bongo Celebrity. Hao wawili walifahamu kuhusu maandishi yangu, wakanishawishi nianzishe blogu. Nami nilifuata ushauri wao.

Nilianzisha blogu mbili: ya ki-Swahili, na ya ki-Ingereza. Nilijifunza na naendelea kujifunza huku nikiblogu. Katika harakati hiyo, Dada Subi, mmiliki wa Wavuti amekuwa akinisaidia, kama anavyowasaidia wanablogu wengine.

Kwangu mimi blogu ni ukumbi wa kuelezea mawazo, hisia, fikra na mambo yangu mengine, na hivi kuyahifadhi na kuwashirikisha wengine. Siblogu kwa imani kuwa nina ujuzi au busara kuliko watu wengine. Blogu ni baraza inayonikutanisha na wengine kwa mazungumzo, mijadala na kubadilishana mawazo.

Vile vile, ninablogu kwa sababu nimeona umuhimu wa blogu kwa upande wa lugha. Ninavyoandika ki-Swahili najiongezea uzoefu wa kutumia lugha hiyo ipasavyo. Hiyo ndio jitihada yangu, na hili ndilo lengo langu.

Mazoezi ni mazoezi. Tunapofanya mazoezi ya viungo daima, tunajijengea afya bora, na tunaanza kuusikia mwili ukikaa sawa. Kwa namna hiyo hiyo, kuandika kwa ki-Swahili kumenifanya niisikie akili yangu ikizidi kukaa sawa, kwa upande huu wa matumizi ya lugha. Nazidi kujiamini katika utumiaji wa lugha hii.

Katika blogu yangu ya ki-Ingereza, naandika kwa lengo la kuonyesha uandishi bora wa ki-Ingereza. Ni lugha ambayo nimeipenda tangu nilipoanza kujifunza, darasa la tatu, na naifundisha hapa katika Chuo cha St. Olaf, Minnesota.

Kublogu kumeniunganisha na watu wengi ambao wanasoma blogu zangu, kutoka pande zote za dunia. Inaleta faraja, kwa mfano, ninapotambua kuwa kitu fulani nilichoandika katika blogu kimekuwa ni msaada kwa mtu fulani. Kwa mfano, miezi kadhaa iliyopita, nilipata ujumbe kutoka kwa mama mmoja aliyeko Ujerumani.

Aliulizia namna ya kufika Mbamba Bay na mahali pa kulala akishafika kule, kwani alikuwa anapangia kuja Tanzania. Alisema kuwa aliniuliza kwa vile alisoma habari za Mbamba Bay kwenye blogu yangu. Nilimpa maelezo aliyohitaji. Wakati huu wote yeye alikuwa Ujerumani na mimi nilikuwa Marekani. Alikuja Tanzania mwaka huu na familia yake, wakati nami niko nchini. Tulionana Ubungo, kwenye kituo cha mabasi, kama inavyoonekana katika picha hii, wakiwa wamefurahi kununua nakala ya Matengo Folktales.

Saturday, February 6, 2010

Wamarekani Safarini Malawi

Leo nilikwenda mjini Chippewa Falls, katika jimbo la Wisconsin, umbali wa maili 123 kutoka Northfield, ambapo naishi. Nilienda kuongea na kikundi cha wa-Marekani wanaojiandaa kwenda Malawi kwa shughuli za kujitolea. Nilialikwa na Mama Diane Kaufmann, ambaye anaonekana kushoto kwangu, katika picha hapa juu. Yeye ameenda Malawi mara kadhaa, katika wadhifa wake kama mratibu wa mpango wa ushirikiano baina ya dayosisi ya Kanisa la kiLuteri Kaskazini Magharibi ya Wisconsin na Malawi. Ana uzoefu wa kupeleka vikundi vya wanadayosisi Malawi katika mpango huo. Vile vile tumeshirikiana kwa miaka kadhaa katika kuendesha mafunzo kwenye kituo cha Luther Point.
Kikundi nilichoenda kukutana nacho leo kinaenda Malawi kuwashughulikia watu wenye matatizo ya macho, na kuwagawia miwani. Wanatarajia kufanya shughuli hizo Karonga na Chitipa.
Baadhi yao wameshaenda Malawi, na kwa wengine hii itakuwa ni mara yao ya kwanza. Mama Kaufmann aliniita niongee nao kuhusu masuala ninayoongelea katika kitabu changu cha Africans and Americans. Alinieleza kabla kuwa washiriki wote watakuwa wamekisoma kitabu hiki kabla ya ujio wangu. Kama kawaida, mazungumzo na watu waliojiandaa namna hii yanakuwa ya kina, kwani yanalenga katika kufuatilia yale ambayo wamesoma.
Walifurahi kuwa nami, kwani walijisikia kama vile wameshanifahamu, kutokana na ninavyojieleza kitabuni. Nami nilifurahi kuwa nao na kuwasisitizia mambo ya msingi kuhusu kuishi au kushughulika na watu wa utamaduni tofauti na wetu. Kwa vile hao wanaenda kwa shughuli za matibabu, mazungumzo yetu yalilenga zaidi kwenye hali halisi ya kushughulika na watu katika hospitali. Tofauti za tamaduni zinajitokezaje katika mazingira ya hospitali.
Kwa bahati nzuri haya ni mambo ambayo nimeyawazia kwa muda mrefu, na katika kitabu changu nimeyagusia. Vile vile, nimekuwa nikijipatia uzoefu katika mazungumzo na wanafunzi wa masomo ya uuguzi wanapojiandaa kwenda Tanzania kimasomo.

Baadhi ya wasafiri hao walisoma katika chuo cha St. Olaf, na tulipata fursa ya kuongelea na kupiga soga kuhusu maisha chuoni hapa. Baadhi wamesoma maandishi yangu mengine, kama vile Matengo Folktales na Notes on Achebe's Things Apart. Niliona wazi kuwa hao ni watu makini ambao wanajishughulisha kufahamu habari za huko waendako.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...