29 September 2005

Juma la kushereheka bagamoyo.

Kila mwaka katika mwezi wa tisa Chuo cha sanaa bagamoyo huandaa tamasha kubwa la sanaa pengine kuzidi yote ambayo hujiri nchini Tanzania. Kipindi hicho ndio kimewadia tena, tamasha hilo lilianza tarehe 27 septemba na litamalizika tarehe 1 Oktoba. Ujumbe wa mwaka huu ni SANAA KWA UTAWALA BORA. Bofya hapa upate undani zaidi wa tamasha hili na habari za chuo kwa ujumla.

27 September 2005

Upendo ni kila kila kitu.

Upendo ni kupenda. Unapopenda kitu hutaki kitu kile kipate madhara ya aina yoyote yale, na pale inapotokea kitu hicho kukumbwa na tatizo basi utafanya juu chini kuhakikisha unatatua tatizo hilo. Mwanao akiumwa utafanya juu chini kuhakikisha anarudia afya yake ya kawaida, unapogombana na Joe Tungaraza wako (mwandani) basi utahakikisha mambo mnayaweka sawa muda si mrefu hii yote ni katika kutaka kuishi kwa raha. Waswahili husema "penye upendo hapaharibiki neno".

Siku zote nimekuwa nikijiuliza ni kwa nini kuna vita, kwa nini kuna matabaka katika jamii zetu, kwa nini kuna rushwa, kwa nini kuna wivu usiokuwa wa maendeleo katika jamii zetu , kwa nini kuna migogoro isiyoisha.. Nimekaa nimefikiria sana na sasa nimepata jibu moja kwamba ni sababu ya ukosefu wa upendo.

Sisemi kwamba kwenye upendo migogoro haitokei hasilani..hapana migogoro hutokea lakini haidumu kwa muda mrefu na kuwa tatizo sugu. Sehemu yoyote yenye upendo watu hujaliana na kuthaminiana, humpenda mwenzie kama anavyojipenda yeye katu hatataka jirani yake apatwe na baya lolote na kama ikatokea mmoja akakumbwa na tatizo basi husaidiana kulitatua. Na huu ndio upendo wa kweli.

Sasa hivi tulio wengi hatuna upendo kabisaaa, si viongozi wa nchi, si raia si yeyote yule. Watu tumegeuka wabinafsi tunajipenda wenyewe tu, kama mtu mambo yako yakiwa swafi basi uhangaiki na mwingine kujua siku imemuendeaje, labda hakula au anauguliwa wewe hujui maadamu siku yako imepita vizuri yeye atajaza mwenyewe. Tukija kwa viongozi wetu....ma-ma-ma-maaa yaani hao ndio usiseme kabisa, kwa jinsi ninavyojua viongozi ndio kama wazazi wetu, husimama badala yetu sisi kama watoto wao na kuhakikisha hatupati matatizo yoyote kuanzia chakula, mavazi, malazi na mienendo ya tabia zetu. Lakini cha ajabu wazazi wetu hawa wamekosa upendo kabisa kwetu sisi watoto wao, wanakula wenyewe kwanza halafu ndio watoto, watoto wasiposhiba wenyewe hawajali, hawajui watoto wamelalaje au wameamkaje, wameenda shule au hawakwenda au wameacha kabisa hiyo wenyewe hawajui wanachojua ni kujishindilia wenyewe basi. Na mimi hili halinishtui kuona kwa nini watoto nao wanaamua kujiingiza katika makundi ya ujambazi na unyakuaji au tabia zozote potofu yote hii ni katika kujaribu kujisaidia maana wazazi wao hawajali. Ndio ni kweli watoto hujifunza kutoka kwa wazazi wao na kama mzazi haonyeshi upendo kwa wanae, watoto watajifunzaje upendo wa kumjali jirani yake?

Tanzania tuna watoto wengi wenye vipaji vya hali ya juu sana, lakini tunashindwa kuwaendeleza watoto wetu kwa vile vipato vyetu viko chini, na hatuwezi kumudu gharama za kuwalipia masomo. Sawa ni kweli lakini bado najiuliza hawa viongozi wetu wenye akaunti zao nchi za ulaya wanashindwa nini kujitolea angalau kila mmoja achukue watoto wawili tu na kuwasomesha? nina hakika hawatapungukiwa na kitu na huo ndio upendo ninaouongelea, hebu fikiria hawa matajiri wote wa Tanzania unaowafahamu wajitolee kusomesha watoto wasio na uwezo wa kifedha katika mashule yao ya akademiki ingekuwaje, nina hakika hawa watoto wasingechezea bahati wangeitwa John visomo. Na ni katika watoto hawa ndio tungepata vijana madhubuti wa taifa la kesho, tofauti na wengi wa watoto wa matajiri waliokulia katika fedha hawana shida ya kujishughulisha sana na masomo kwani fedha ipo na wanafikiri itakuwepo milele.

Haya, mimi sina mengi ya kusema lakini akili yangu inanituma kusema kwamba kama watanzania tutarudisha upendo kati yetu basi mabalaa yooote yanayotufuata fuata yatatafuta njia ya kutokea.

16 September 2005

Mbona tunamuacha peke yake??

Kina mama sasa sijui hata tunataka nini, tumelia sana juu ya usawa wa jinsia,tuwe na haki sawa na wanaume, nasi tutambuliwe na kuthaminiwa kama wanaume. Yote tumeyapata sasa kijasho chembamba kinaanza kututoka, tunaogopa nyadhifa za juu hususani uongozi wa nchi, suala la kutokujiamini linarudi palepale. Sawa yote tisa...kumi...basi hata mmoja wetu anapojitokeza tunashindwa hata kumuunga mkono!!! loooh kazi bado tunayo. Dunga hapa ujisomee mwenyewe.

15 September 2005

Hawatakaa wasahau.......

Ni mchana tulivu kabisa shuleni Nganza sekondari, wakati huo nikiwa kidato cha nne na mdogo wangu Mama Oprah kidato cha tatu. Tumekaa darasani tukijisomea huku tukisubiri kengele ya chakula igongwe wasichana tukapate ugali maharage, mara badala yake tunaona darasa zima la kina Mama Oprah linatolewa nje na kupigishwa magoti uwanjani, punde si punde ofisi nzima ya waalimu inatoka kila mwalimu akiwa na fimbo kadhaa mkononi...... heee! kulikoni tena mbona form three wamefanya nini?

Kisa chenyewe ndio hiki..., Mwalimu ???(wa kiume) alikuwa darasani akifundisha kama kawaida, Mwalimu huyu ukimwangalia tu utasema sijui aliumwa nini alipokuwa mtoto, uso wake una vijishimo vidogo na vikumbwa, ugonjwa huu uliompata utotoni ulimuathiri hadi ulimi wake ukawa mzito kuongea inabidi umzoee ili umwelewe kwa wepesi.

Sasa wanafunzi darasani, njaa imeshawakamata masikini ya Mungu, hawamsikilizi tena mwalimu bali wameanza kumkagua juu hadi chini. Mmoja akakata kikaratasi akaandika kitu fulani, akampasia mwenzie chini ya deski, akasoma akacheka kwa chini chini, akampasia na mwingine naye hivyo hivyo baada ya kusoma akacheka na kumpasia mwenzie, kazoezi haka kaliendelea bila mwalimu kujua kitu chochote, wanafunzi sasa karibu wote wanacheka chini chini, mwalimu akastukia kitu lakini akauchuna na kuanza kuwategea ili kujua ni nini kinachoendelea... watoto nao bila kujua wanaendelea kupasiana kikaratasi....mara ghafla mwalimu akamnyaka mmoja akimpa mwenzie....hapo hapo mwalimu akakiomba kikaratasi... akapewa yaani hapo darasa zima ni kama limemwagiwa maji... mwalimu akasoma kikaratasi looooh!! kinasema "uso wa mwalimu??? kama nyama ya ini". Jazba iliyompanda pale sipati kusema alitoka nje moja kwa moja ofisini akawakabidhi waalimu wenzie wasome....kilichoendelea hapo Bugando hospitali ndo inajua...... zilipita fimbo balaa ......lilikuwa ni fundisho.

12 September 2005

Hatukujitokeza.

Bado tunasua-sua kina mama katika kutaka kushika usukani wa kuiongoza nchi yetu. Kama inavyojulikana kwamba mwezi ujao ndio uchaguzi mkuu wa kumchagua dereva wa nne wa kuikamata nchi yetu, ni mwanamke mmoja tu aliyejitokeza kugombea nafasi hiyo, tena si kwa kupenda mwenyewe bali ni kwa vile hakuna mwanamke aliyejitokeza. Yeye mwenyewe anakiri kwamba kama wanawake wakongwe kwa siasa wangegombea basi yeye katu, asingedhubutu kugombea,lakini kwasababu wamegwaya basi hakuwa na jinsi. Huyu si mwingine bali ni bibi Anna Claudia Senkoro. Lakini pamoja na hayo tunampongeza kwa uthubutu wake, amefungua njia.

Nilikuwa naongea na mshikaji wangu mmoja,juu ya suala hili la uongozi wa nchi kwa wanawake, akasema ingependeza sana na kungetokea mabadiliko makubwa kama Tanzania ingeongozwa na upande wa pili wa shilingi, akasema ukitaka kujua mwanamke hateteleki katika masuala ya uongozi basi mwangalie jinsi anavyoiongoza nyumba yake, tena tafuta yule mwanamke ambaye ana mume jina, ambaye akitoka leo uhesabu siku tatu ndo utamuona. Mwanamke huyu kwa vile ameshajua hana msaada wowote, basi atafanya kila aliwezalo kuhakikisha mambo hayaharibiki wa kuadhirika, mtakula, mtavaa na mtasoma. Akasema kwa ufupi mwanamke si mbinafsi, hufikiria kwanza watu wake halafu ndio yeye. Kwa hiyo kama mwanamke huyu akikamata madaraka ya kuiongoza nchi hatashindwa kwa vile ameumbwa na utu na uwezo wa kuongoza.

Nikamuuliza mbona kuna wanawake wengi ambao wanaongoza hadi sasa lakini hatuoni badiliko lolote ?...akasema hao wako chini ya vivuli juu yao kuna wanaorekebisha mambo, lakini kama kweli mwanamke mwenyewe ndio akawa Top macho yote yanamwangalia yeye basi ndo utamjua.

Nikamuuliza tena kwamba pamoja na sifa zote hizo za uwezo wa kuongoza kwa mwanamke, lakini bado kuna huu udhaifu wa kuona huruma na woga wa kuyakabili matokeo ya siasa kama kwenda jela na vitu kama hivyo... akasema hilonalo ni tatizo kubwa maana siasa ni kujitoa muhanga hasa, ni lazima uwe na roho kama ya malkia Sheeba au malkia Nzinga.

Baada ya maongezi hayo, binafsi nikaanza kupata picha, ya kwa nini tunasita sita katika kukamata madaraka ya juu, kwamba tunasumbuliwa na uzuri, hatutaki kuaibika, kuzomewa wala kukataliwa...aibu hiyo itupitie mbali kabisaaa, pili hatutaki kuteseka kama kwenda jela pale utakaposema ukweli.

Kina mama hebu tukae na tujiulize tena na tena,hadi lini tutakuwa tukisumbuliwa na tatizo hili la woga na kujipenda mno? Ninaamini nguvu ya uongozi tunayo sema hiyo minyororo ya utumwa tuliyojifunga wenyewe ndo inatumaliza.

Jamani tusaidianeni kuifungua tuwe huru.