23 May 2005

Malkia Nzinga Mbande wa Angola.


Kama ukibahatika sasa hivi kukutana na Mreno, wewe jifanye kama unamchokoza juu ya wanawake wa afrika kwamba hawana lolote na hawawezi lolote, uone atakavyokushangaa, na bila shaka atakutupia swali kwamba unaishi dunia gani wewe?

Wasomaji msishangae, kwani aisifiae mvua...imemnyea. Hii yote imetokana na mwanamke mmoja jasiri, shupavu, mwenye akili sana na asiyetaka kuonewa wala kudharauliwa, si mwingine ni Malkia Nzinga Mbande. Mwanamama huyu aliyezaliwa mwaka 1583 na kufa 1663, alikuwa ni mtoto wa chifu na aliishi kipindi ambacho biashara ya utumwa ndio ilikuwa imepamba moto kwelikweli, kwa bahati mbaya baba yake alifariki na hivyo kaka yake mkubwa bwana Ngola Ngoli Mbandi akarithishwa madaraka ya baba yake. Mm! kaka huyu bila shaka aliguna kwa kujua kabisa kasheshe analotakiwa alikabili la kuwazuia wareno kuingia nchini kwao, lakini afanyeje na yeye ndio mwanaume na kama inavyojulikana kwa wengi mwanaume anaweza kila kitu na daima si mwoga, ikabidi ayavae madaraka huku akijua kabisa yeye ubavu wa kukabiliana na wareno hana na ni
mwoga kufa.

Dada yake, Nzinga baada ya kuona kaka yake anasua-sua ikabidi amwambie, kaka ni lazima uchukue hatua juu watu hawa na kuwazuia kuingia kututawala, lakini kwa vile kaka yake alikuwa mwoga ikabidi amwombe dada yake amsaidie, mara moja bila kuchelewa mwana mama Nzinga akaanza kuchukua hatua za utekelezaji na akafanikiwa kuwashawishi wareno katika kuandika mkataba wa makubaliano ya amani.

Tarehe ikapangwa ya kuweka saini makubaliano hayo, Kaka mtu kwa woga akakataa kwenda hivyo ikabidi Nzinga amwakilishe, akaenda na watumishi kadhaa lakini walipofika ndani ya ukumbi Nzinga akagundua kwamba hakuwekewa kiti yeye kama kiongozi wa nchi yake isipokuwa gavana wakireno peke yake, mwanamama akaona dharau gani hii? mara moja akapiga kofi na mmoja wa watumishi wake akaja mbele yake na kuinama magoti na mikono chini, Nzinga akakaa juu yake, kwa hiyo suala la gavana kukaa kwenye kiti peke yake likawa ngoma droo. Gavana akamtizama yule mama bila kummaliza na kubaki na aibu ya kuzidiwa maarifa tena na mwanamke, bila shaka alibaki akijiambia duh! kumbe wanawake nao wamo!!!

Nzinga baada ya kugundua kwamba kaka yake si kiongozi mzuri na hawezi kila kitu, alimfunga na kujitangaza kwamba yeye ndiye atakayeshika nchi kinyume na desturi ya nchi yao kwamba mwanamke haruhusiwi kushika wadhifa wowote wa uongozi katika serikali, minong'ono ya hapa na pale ilitokea lakini haikufika mbali kwani Nzinga alithibitisha ujasiri wake kwa vitendo. Na ni hapo ndipo umalkia wake ulipoanzia.

Kwa muda wa miaka arobaini ya uongozi wake, wareno walishindwa kuitwaa Angola hadi alipofariki, mwanamama huyu alijulikana na kuogopwa sana na ulaya nzima kwa mbinu zake thabiti za kijeshi, alijulikana kama mwanamke mpiganaji, jasiri na mwenye akili.
Hebu fikiria wareno, pamoja na kuwa na silaha imara na za kisasa ukilinganisha na za Malkia Nzinga, lakini walishindwa kuiteka Angola hadi Malkia Nzinga alipokufa.

Huyu kweli ni mwanamke wa shoka, na nina amini kila mwanamke anaweza kuwa mwanamke wa shoka, pale atakapoamua kufanya jambo kwa moyo na kuondoa uwoga. Hapa duniani kila jambo linawezekana, tatizo liko kwetu sisi wenyewe kutanguliza woga na kutokutaka kusumbuka.

HAYA HIMA HIMA KINA MAMA.

20 May 2005

Huyu ndiye mwanamke wa shoka.

Sifa hizi za mwanamke wa shoka nimezipata katika maandiko matakatifu ya wakristo katika kitabu cha Mithali 31:10-31. Zinasema hivi:-

Mke mwema ni nani awezaye kumwona?
Maana kimachake chapita kima cha marijani.
Moyo wa mumewe humwamini,wala hatakosa kupata mapato.
Humtendea mema wala si mabaya, siku zote za maisha yake.
Hutafuta sufu na kitani,hufanya kazi yake ya mikono kwa moyo.
Afanana na merikebu za biashara,huleta chakula chake kutoka mbali.
Tena huamka kabla haujaisha usiku,
Huwapa watu wa nyumbani mwake chakula, na wajakazi wake sehemu zao.
Huangalia shamba akalinunua, kwa mapato ya mikono yake hupanda mizabibu.
Hujifunga nguvu viunoni kama mshipi, hutia mikono yake nguvu.
Huona kama bidhaa yake ina faida, taa yake haizimiki usiku.
Hutia mikono yake katika kusokota, na mikono yake huishika pia.
Huwakunjulia maskini mikono yake, naam huwanyooshea wahitaji mikono yake.
Hawahofii theluji watu wa nyumbani mwake, maana wote wa nyumbani mwake huvikwa nguo nyekundu.
Hujifanyizia mazulia ya urembo, mavazi yake ni kitani safi na urujuani.
Mume wake hujulikana malangoni, aketipo pamoja na wazee wa nchi.
Hufanya nguo za kitani na kuziuza, huwapa wafanyabiashara mishipi.
Nguvu na hadhi ndiyo mavazi yake, anaucheka wakati ujao.
Hufumbua kinywa chake kwa hekima, na sheria ya wema i katika ulimi wake.
Huangalia sana njia za watu wa nyumbani kwake, wala hawali chakula cha uvivu.
Wanawe huondoka na kumwita heri, mumewe naye humsifu na kusema,
Binti za watu wengi wamefanya mema, lakini wewe umewapita wote.
Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili,
Bali mwanamke amchaye Bwana ndiye atakayesifiwa.
Mpe mapato ya mikono yake, na matendo yake yamsifu malangoni.

15 May 2005

Mkombozi wa mwanamke ni elimu.

Nakumbuka enzi zetu za Nganza sekondari, ambapo wengi wetu tulikuwa tukiuchezea wakati kwa madai kwamba kuna wanaotusomea. Utakuta mwanafunzi anakacha vipindi vya masomo na kujificha bwenini bila sababu yoyote ukimuuliza atakwambia...achana na mimi mwenzio nasomewa, utakapohoji zaidi atakwambia nyie hangaikeni tu, lakini mjue mwanamke mwisho wake ni kuolewa, kuzaa na kulea wanae sasa kwa nini nijisumbue?

Enzi hizo dhana hii, nilikuwa nikiichukulia juu juu, sikuwahi kabisa kukaa na kuitathmini kiundani nini faida na madhara yake, nina hakika haina faida hata kidogo kwani matokeo yake sasa yanajionyesha waziwazi kabisa, kwa mfano tukiangalia suala la ujasiri na uthubutu wa kufanya jambo kati ya mwanamke na mwanaume, tunaona kwamba kuna tofauti kubwa sana, kama ni nafasi kumi zimetolewa, basi utakuta wanaume saba na wanawake watatu au hata chini ya hapo. Na hii si kwa sababu wanawake wamezaliwa hawawezi bali ni kutokana na mbegu iliyopandwa siku nyingi vichwani mwao kwamba wao ni wa kusomewa hivyo wasubiri tu. Na ni hapa ndipo ninapoona maana ya ule usemi usemao utavuna ulichopanda, wanawake sasa hivi tumebaki tukilalamika kwamba tunaonewa na wanaume,...kwamba kwanini kiuwiano wanaume ndio wameshika nafasi zilizo nyingi na za juu kimadaraka,....lakini hebu tuangalie ule ukweli wanawake wenzangu, hivi hizi nafasi wanapeana tu bila ya kuwa na kitu kichwani??....tukumbuke ule wakati wa kuingiza vitu kichwani tulivyokuwa tukiuchezea, na haya ndio matokeo yake.

Kwa upande wa wanaume, wao nao enzi hizo kwa kujua wanasomea watu, basi walijitahidi kwa kila njia kusoma wakijua kuna majukumu mazito ya kuisimamia familia, na hii ndio imewafanya wawe jasiri na wenye uthubutu, kwa sababu mbegu iliyopandwa kichwani mwao ni ya kupambana. Na bahati mbaya zaidi hata hao waliokuwa wakitusomea wameshtuka, hawataki mambu-mbu-mbu.

Jambo la kujifunza hapa wanawake wenzangu, ni kuanza kushughulika na mizizi na si matunda, ukikata mizizi matunda hayataendelea kuzalika na mti hauna ujanja tena utakufa tu. Na mti ukishakufa tunapanda mpya kwa makini zaidi. Ni lazima tuiweke elimu mbele, ni lazima tujifunze uvumilivu wakati wa kuipata hiyo elimu na hapo ndipo ndipo mambo yatakaposawazika yenyewe bila hata kuyapigia mbiu.

12 May 2005

Utukutu wa chama.

1. Chama chetu kimetuongoza, hadi uhuru tulipoupata,
Kinaendelea kuongoza, kufikia lengo umoja,
Mwenyekiti Mwalimu Nyerere, mwenye hekima na wingi wa sifa,
W: Tanzania.

Ewe chama chombo chetu madhubuti kabisa,
Ndio wewe nguzo, muokozi wa taifa,
Mwenyekiti Mwalimu Nyerere mwenye hekima na wingi wa sifa,
W: Tanzania.

2. Kwa wasafiri wenye busara, ni wajibu wao kukumbuka,
Wafikapo safari salama, hata njiani bado wakiwa,
Kulinda chombo chao vyema, pia nahodha kumshikilia,
W: Tanzania

3. Ulifika wakati mgumu, wananchi walifadhaika,
Utumwa ukoloni ni sumu, sisi sote tulihangaika,
Ni wajibu wetu kushukuru, Nyerere alipojitokeza,
W: Tanzania.

4. Chama chetu kweli ni ngome ya chuma, sisi sote tunazingatia,
Mwalimukiongozi wa umma, nani twaweza kumlinganisha?
Ametutoa katika utumwa, wananchi sasa tnalinga.
W: Tanzania.

NCHI YANGU ENZI HIZO...

09 May 2005

Hivi tumerukwa.....??

Kuna jambo moja ambalo mara nyingi silielewi, hivi ni kwa nini waafrika tulio wengi tumekubali kujishusha namna hii? kiasi kwamba tunawasaidia wenzetu hawa weupe kuwapa chati bila woga hata kidogo. Majuzi nilikuwa na rafiki yangu tukitembea mitaani, kwa kweli mitaa tuliyokuwapo hairidhishi kiusafi hata kidogo, vinyesi, harufu na ramani za mikojo kutani, makaratasi yamesambaa ovyo, na mengine mengi. Rafiki yangu akaanza kwa kuguna..mh! utadhani tuko Afrika...hataa hii si bure lazima sehemu hii wakazi wake ni watu weusi, nikamuuliza kwa nini unasema hivyo, ina maana yaliyo mazuri yote ni ya wazungu na mabaya yote ni ya waafrika? akasema bwana eeh, hawa wenzetu wametuacha sana, hata iweje hatutakaa tuwapate....Hakyanani niliishiwa la kusema ila nikamkumbusha usemi usemao 'usipojidhamini ni nani atakuthamini?'

Hali hii imenikumbusha tabia ya waafrika walio wengi waishio ughaibuni kutokutaka kupiga picha kabisa katika maeneo mabovu mabovu, utasikia wanasema, watajuaje kama niko majuu bwanaa?? piga picha hata ukipeleka kwenu picha yenyewe inajieleza.
Jamani tubadili tabia hii, ni lazima ukweli uwe ukweli kwani kwa tabia hii tunajishusha wenyewe na kuwapandisha wenzetu, mbona wenyewe wakija kwetu wanakwepa kupiga picha mambo mazuri?? tujiulize hilo...ukweli bado uko pale pale si maeneo yote ya ughaibuni ni mazuri, na si maeneo yote ya Afrika na mabovu.

MKOMBOZI WA MWAFRIKA NI MWAFRIKA MWENYEWE.

08 May 2005

Ngo...ngo...ngo..hodiii!

Ngo...ngo..ngo... hodiii, jamani wenyewe mpoo?...inaelekea wametoka, ngoja niache ujumbe mlangoni.

Wanablogu,
Nilipita kwenu lakini inaelekea hamkuwepo, nia hasa ilikuwa nikuwapa taarifa kwamba nami nimeingia katika ulimwengu wa blogu. Blogu yangu itajulikana kwa jina la Da'Mija, Da mija atakuwa akizungumzia masuala ya jamii na mabadiliko yake ya kila siku. Atafundisha atakapoona panafaa kufundisha, atajadili pale atakapoona panafaa kujadili, atatoa mawazo pale atakapoona panafaa kutoa mawazo na mengine mengi yatajitokeza kulingana na siku zitakavyokuwa zikienda.

Asanteni.